Popular Posts

MICHEZO

Sunzu awashangaa Samatta, Ulimwengu

BEKI wa timu ya Taifa ya Zambia na TP Mazembe, Stopila Sunzu ameshangwa na kitendo cha washambuliaji wa kimataifa wa Tanzania wanaocheza timu ya TP Mazembe, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu kushindwa kujiunga na timu ya Taifa.
Akizungumza na Mwananchi jana, Dar es Salaam, Sunzu alisema timu ya taifa ndiyo daraja la mafanikio kwa mchezaji yoyote duniani kwa sababu, ubora wa mchezaji hupimwa kwa mambo mengi na mojawapo ni mchango wake kwenye timu ya taifa kwa mechi za kirafiki na mashindano.
“Hata mimi nilitegemea kukutana nao katika mechi hii, lakini sifahamu kwanini hawajacheza labda ni majeruhi ndiyo maana wameshindwa kucheza,” alisema.
Aliongeza: “Kama hawakuwa majeruhi watakuwa wamefanya makosa makubwa kwa sababu mechi kama hizi zinafuatiliwa na watu wengi sana ikiwemo Shirikisho la Soka Afrika (CUF).”
Kuhusu suala la nidhamu ya wachezaji hao Sunzu alisema kwamba wakiwa TP Mazembe ni watu wenye nidhamu nzuri na wanajituma kwenye mazoezi na hata kwenye mechi ndiyo maana wanapata namba.
“Moja ya sera muhimu ya TP ni nidhamu kabla ya uwezo wa mchezaji na ukikosa nidhamu unaweza kukosa namba.”
Akizungumzia suala la majeruhi, alisema wakati wanaagana Congo DRC, hakufahamu kama wachezaji hao ni majeruhi. “Kuna wakati mchezaji anaweza akawa majeruhi, lakini akajikaza kutokana na umuhimu wake kwenye timu na umuhimu wa mechi,” anasema.
Naye Kocha Mkuu wa timu ya Taifa, Kim Poulsen amesema kuwa wachezaji wasiokuwa na moyo wa kuichezea timu ya Taifa hawatapata nafasi hata kama watakuwa na uwezo kiasi gani.
Kim alisema hayo mara baada ya kuombwa kutoa maoni yake kufuatia Samatta na Ulimwengu kuzomewa na mashabiki wakati wa mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Taifa Stars na Chipolopolo ya kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi.
Kocha huyo raia wa Denmark alisema hana maoni kuhusiana na suala la kuzomewa kwa Samatta na Ulimwengu, ambao mara kwa mara wanakutana na vipingamizi wanapoitwa kuichezea timu ya taifa.
“Sitaki kuwasemea mashabiki kuhusiana na suala hilo, lakini wao wanajua nini walichokifanya, ila nimeweka utaratibu mwingine wa kufanya kazi.
Sihitaji mchezaji asiyekuwa na moyo na timu,” alisema Kim.
Alisema kuwa anajua itachukua muda ili kuweza kupata timu imara, lakini katika mpira wa miguu ni jambo la kawaida kwani hata wapinzani wao (Zambia) wana historia hiyo mpaka kufikia mafanikio.
“Nnawapongeza wote. Tulikuwa na wakati mgumu hasa upande wa washambuliaji ambapo ilinibidi kutumia viungo wengi ili kuweza kumiliki mpira na kushambulia kwa kushtukiza, tuliweza kutengeneza nafasi nyingi na kutumia moja, hii ni faraja kwangu na kwa Watanzania wote,” alisema.
Alisema kuwa matokeo ya mechi ya juzi ni makubwa kwa Tanzania, kwani kuifunga timu bingwa katika Bara la Afrika ni jambo la kujivunia. “Hii ni zawadi ya Krismass na Mwaka Mpya kwa wadau wa soka.”

No comments:

Post a Comment